Ni kama kikohozi,
Ndilo nilowasikia wakisema,
Magwiji wa sanaa na mistari,
Nayo lizidisha kuchemua,
Harufu yake ya manukato.

Koo liwasha, mikwaruzo-
Kukohowa ilibidi,
Japo makali kwa vidonge lipunguza;
Ama likuwa kama kohozi,
Langu kwake penzi.

Alinipamba kwa zawadi,
Maji moto pia kanipa,
Japo kulikausha.
Nalo ni kikohozi,
Kulificha mie kashindwa.

Kumbe mwenzangu,
Kwa limau, ‘tungu sumu na tangawizi,
Penzi kazuia, nalo ni kohozi,
Lamlipuka baada ya kitambo,
Mwenzio ‘shanikaukia!

Basi ‘kipenda, penda,
Penzi lauma, ni kama kikohozi,
Ila likisha ni mazoea,
Ni tabasamu la kumbukumbu,
Sizuie uwapo mwasho!