Ana sura na umbo la ajabu, isitoshe macho ya kiarabu.
Nyanja zake si za wenye taabu,
dhambi tele hata akizificha na hijabu!
Ombi lake laudhi, kujitosa hana budi,
kwa uvumba kisha udi, kukubaliwa ndo zake juhudi.
Anaamini na laki,
kwake raha zatamaliki,
kwake, ndo haki..

Sauti zao ndo kwake mizani,
dunia kiutani anaipima uzani.
Ana uraibu ela hana aibu.
Kwake mambo nadhifu,
fujo zenyu kwake hafifu.
Hutamshtaki, kwake ndio haki..

Hataki pingu za maisha, wazo hilo kwake latisha!
Kwa hivyo yupo kizimbani bila hata dirisha, akiomba yataisha.
Pete si kwa lake chanda, heri utamani tu kumpanda.
Wengi kitanzi wanawaza kwa lake penzi mkanda!
Kwake nyuma hatabaki,
kwake ndio haki..

Ana fikra za kutisha.
Kila yuazini yuahisi mumewe yuabisha.
Jamii yuaaibisha, ndoa kuitaifisha, itakuwaje kisha?
Hapawi talaka, yeye ndo yuatalaki,
kwake ndio haki..

Ana chuki binafsi, kafanya mzinga wa nyuki binafsi ndio ale uki binafsi!
Ni mchoyo, hasitiri nafsi. Hafichi, haridhiki basi, tumfanye nini nasi?
Maisha yuapenda kasi, kicheche moto wa pasi. Nimemaka adinasi!

Zake tena sigusi, moyo mweusi, kamusi –
matusi, sifa mbovu kaskazi na kusi!
Havikuanza juzi, nadhani ni upuzi,
kagundua kuna mfupa kwenye mchuzi?
Hataki! Kwake ndio haki..
Mkanda wako ndo wake uzi,
ya kesho yuataka juzi, hisia hazileti mchuzi,
vichekesho ni upuzi, kila neno kwake ni ushuzi!

Utapita na upepo, ashapandwa nazo pepo,
ndoto za mizimwi, moto ni kama hauzimwi!
Maisha kipanya, fikra za kuchanganya.
Hasemezewi, na hata akisema simwelewi!
Haogelei na ni samaki? Sawa, kwake ndio haki..

© jemedari