Eeh nchi yangu, taifa usoambilika,
Wewe ulotokwa na machozi kwa kitambo kirefu,
Uloyapangusa nayo yakazidi tiririka,wala funzo weye hujapata.
Nchi na mama yangu, wewe uujuaye utungu wa kiboko, mshale na upanga,
Waufahamu, mpenyo wa risasi na vitoa machozi
Eeh taifa langu, ujuaye uhalisi wa mbwa mwitu aliyejivaa u’kondoo
Umenyanyaswa kwa kitambo kirefu, kwani sauti yako yafikia mbali bali yakurudia,
Mwangwi waliopigana babu zetu ili usipate kuwarudia wao na vizazi vyao leo,
Wewe ulohifadhi mwako moyoni sauti za kilio na maombolezi;
Za kina mama wakiwalilia wanao na waume waliowaacha,
Za kina baba wakiomboleza maafa yao, na
Vijana wakiomba kuiona furaha ijapo silaha mikononi,
Za watoto wakitazamia kuuona utulivu, na
Wazee wakongwe wakiwalilia wana na wajukuu wao waliofariki
Na kuwaacha wao waking’ang’ana na mikongojo yao inayowalemea kwa uzee,
Tazama, leo siku njema, hamsini miaka watizama nyuma
Kuanzia leo, iwe mimi na wewe, tu ndugu, tu kabila moja,
Tu wana wa mama mmoja, wana wa Kenya.